William Martin, Mfanyakazi wa Maktaba ya Umma ya New York mwenye uzito wa kilo 163 na urefu wa futi 6 na inchi 2, amefungua kesi dhidi ya Mwajiri wake akidai fidia ya dola milioni 4.6 (bilioni 12 za Kitanzania) kwa kumpa dawati dogo kuliko mwili wake na kumsababishia matatizo ya kiafya na kiakili.
Martin, anayefanya kazi kama Msaidizi wa taarifa za Maktaba, alieleza Mahakamani kuwa dawati alilopangiwa kwenye Maktaba ya Stavros Niarchos Foundation lilikuwa dogo, finyu na lenye sehemu inayoyumba, hali iliyomletea maumivu ya mwili na changamoto za kiafya.
Kulingana na Martin, matatizo hayo yalianza mwaka 2021 alipolazimika kutumia Dawati hilo na baada ya malalamiko yake alihamishiwa Dawati lingine kwa muda, lakini Juni 2023 alirudishwa tena kwenye Dawati hilo na Mkurugenzi mpya jambo lililoathiri zaidi afya yake.
Martin pia alidai kuwa alipata tuhuma za uongo za kulala kazini hali iliyosababisha kusimamishwa kazi na kumfanya aombe likizo ya matibabu kwa ajili ya msongo wa mawazo na wasiwasi pia anasema athari za tukio hilo zimemfanya kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Msemaji wa Maktaba ya Umma ya New York alikanusha madai hayo, akieleza kuwa wanazingatia mahitaji ya Wafanyakazi wao kwa haki na heshima. Kesi hiyo bado iko Mahakamani.