Wanawake nchini China wamebainika kutumia ndoa feki kama mbinu ya kujipatia mamilioni ya pesa kupitia ulaghai wa mahari. Mpango huu unaojulikana kama “Ndoa za Haraka” (flash marriages) unahusisha wanawake kujifanya wachumba wa wanaume waliotafuta wenza kupitia mashirika ya upatanishi wa ndoa. Baada ya kufanikisha ndoa, wanawake hao walitoroka au kusababisha talaka kwa makusudi, na mara nyingi wakiwa tayari wameshakusanya kiasi kikubwa cha mahari.
Kwa mujibu wa ripoti za mahakama ya Guiyang, mji wa Guizhou, polisi walipokea zaidi ya malalamiko 180 kuhusu ulaghai wa ndoa katika eneo hilo tangu Machi mwaka jana. Wanawake waliokuwa wakihusika katika ulaghai huo walipata zaidi ya yuan 300,000 (karibu milioni 104 za Kitanzania) ndani ya miezi mitatu tu.
Uchunguzi unaonyesha mashirika haya yalihamisha shughuli zao hadi mikoa jirani kama Yunnan baada ya mamlaka kuanza kuchukua hatua kali.
Njia hii ya ulaghai imeibua mjadala mkubwa, huku wengi wakitilia shaka ongezeko la matumizi ya mitandao na mashirika ya upatanishi wa ndoa kama sehemu ya udanganyifu dhidi ya watu wanaotafuta maisha ya ndoa halisi.