Rais wa Urusi Vladimir Putin, ametishia kuyashambulia majengo ya kufanyia maamuzi ya Kyiv baada ya msururu wa mashambulizi makubwa jana usiku.
Amezungumza kwa mara ya kwanza akiwa katika mkutano wa kilele nchini Kazakhstan na kusema majengo ya kufanyia maamuzi yanaweza kulengwa kwa kombora jipya la balestiki ambalo Urusi ililitumia kushambulia mji wa Dnipro wa Ukraine wiki iliyopita.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi imeshambulia Ukraine kwa makombora 90 na ndege zisizo na rubani 100 usiku kucha kujibu mashambulizi ya Ukraine kwa kutumia silaha za Uingereza na Marekani wiki iliyopita.
“Tumefanya mashambulizi makubwa,” amesema, na kuongeza kuwa vituo 17 vya kijeshi katika eneo la Ukraine vimepigwa.
Amesema Urusi imerusha makombora 100 na ndege zisizo na rubani 466 kwenda Ukraine katika siku mbili zilizopita.
Zaidi ya watu milioni moja nchini Ukraine hawana umeme baada ya Urusi kushambulia mitambo ya umeme ya nchi hiyo katika maeneo kadhaa.