Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa mkono wa pole kwa familia ya mwanamuziki mkongwe wa dansi, Marehemu Boniface Kikumbi “King Kiki” na familia ya Muigizaji marehemu Fred Kiluswa kwa kuwapatia rambirambi ya Shilingi Milioni 10 kila familia.
Rambirambi hizo zimewasilishwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, alipotembelea familia hizo akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Taasisi ya mama Ongea na mwanao, Steve Nyerere, Asha Baraka, Muandaaji wa filamu William Mtitu na Ignus Mkindi leo Desemba 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
“Kama tulivyoshirikiana kipindi cha kuuguza, Serikali imeona ni vyema kuendelea kuwashika mkono hata kipindi hiki cha majonzi, yaliyotokea ni mipango ya Mungu hatuna budi kuikubali lakini tunawaahidi kuwa tutaendelea kuwa pamoja” amesema Mhe Mwinjuma.
Marehemu King Kiki, ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 15, 2024, anakumbukwa kwa mchango wake katika muziki wa dansi, ambapo alitamba na nyimbo mbalimbali maarufu, ikiwemo “Kitambaa Cheupe.”
Vilevile marehemu Fred Kiluswa aliyefariki dunia Novemba 16, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mloganzila atakumbukwa kwa namna alivyokua anafanya vizuri katika filamu.