Serikali ya Uingereza imepanga kupiga marufuku matangazo ya Televisheni ya Vyakula vyenye sukari nyingi kama vile burgers, muffins na vyakula vingine vinavyosadikika kama vyakula vibaya kwa afya (junk food) kwa lengo la kupambana na ongezeko la uzito mkubwa kwa Watoto ambapo marufuku hiyo ikitarajiwa kutekelezwa kuanzia mwezi Oktoba 2025.
Hatua hii inatokana na ripoti kutoka Huduma ya Taifa ya Afya (NHS) Nchini humo inayosema kuwa karibu Watoto 1 kati ya 10 walio na umri wa kuanza Shule wanakabiliwa na tatizo la uzito mkubwa na takribani asilimia 23.7% ya Watoto wa miaka mitano wanakabiliwa na kuoza kwa meno kutokana na ulaji wa sukari nyingi ambapo Waziri wa Afya Wes Streeting alielezea kuwa sera hii ni hatua ya kwanza kuelekea mabadiliko makubwa ya huduma za afya kutoka kwa kutibu Magonjwa hadi kwa kuzuia Magonjwa na kuwapa Watoto afya bora.
Vyakula vingine vilivyomo kwenye orodha ya Vyakula vilivyokatazwa ni pamoja na keki, vitafunwa, vinywaji vya nishati ( energy drinks) na vyakula vingine vyenye sukari, mafuta na chumvi nyingi, hata hivyo Vyakula vya asili kama shayiri ya asili na Mtindi vimeachiliwa kutangazwa ikielezwa kuwa Serikali ya Uingereza inatarajia kupunguza kesi za uzito mkubwa kwa Watoto zaidi ya 20,000 kila mwaka kwa hatua hii na kuahidi kupunguza kalori 7.2 bilioni kutoka kwa lishe za Watoto kila mwaka.
Serikali ya Uingereza inatumaini kuwa hatua hii itasaidia kupunguza ongezeko la uzito mkubwa kwa watoto na kuwaepusha na matatizo ya kiafya kwa baadaye.