Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke mnamo tarehe 3 Disemba, 2024 wamefanikiwa kumfanyia upasuaji Mwanamke mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa mkazi wa Dar es salaam na kuondoa uvimbe wenye Kilogramu 7 kwenye mfuko wa mayai wa upande wa kulia uliomtesa kwa miaka 15 na kumsababishia kushindwa kushika ujauzito
Upasuaji huo umeongozwa na jopo la Madaktari Bingwa watatu (3) kutoka Hospitali ya Temeke akiwemo Dkt. Joseph Kiani, Dkt. Abdallah Mashombo pamoja na Dkt. Ikra Abdallah wote wakiwa ni Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi wakisaidiwa na wauguzi Liliani Patrini na Joseph Petro pamoja na Wataalamu wa usingizi Rashidi Dadi, Selemani Selemani na Eva Kuziganika
Akizungumzia upasuaji huo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Temeke Dkt. Ikra Abdallah amesema uvimbe huo wenye kilogramu 7 umetolewa katika mfuko wa mayai wa upande wa kulia wa mwanamke huyo ambaye alikuwa akisumbuliwa kwa zaidi ya miaka 15 na kushindwa kushika ujauzito
“Mwanamke huyu alikuwa anasumbuliwa na ongezeko la ukubwa wa tumbo ambapo kwa macho alikua anaonekana kama ni mjazito na tumbo lake lilikuwa kubwa kama la mama mjazito Mwenye watoto mapacha, pia licha ya kuwa na uvimbe huo mkubwa tumbo lake lilijaa maji kiasi kama cha Lita 4 ambapo baada ya kumfanyia uchunguzi tukaona sio uvimbe wa kawaida ndipo tukamfanyia upasuaji na tumefanikiwa kutoa uvimbe wenye kilogramu 7 kwenye mfuko wa mayai na uvimbe huo tumeupeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya uchunguzi zaidi”, Alisema Dkt. Ikra Abdallah Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na uzazi
Dkt. Ikra Abdallah anatoa ushauri kwa jamii hasa wanawake unapoona changamoto yoyote katika mfumo wa uzazi ni vizuri kufika Hospitali mapema kwaajili ya uchunguzi na matatibabu kwasababu wengi wenye matatizo ya uvimbe mkubwa kwenye kizazi ni wale ambao mara nyingi wanachelewa kufika Hospitali ili kupatiwa tiba hivyo unapoona dalili zozote za tofauti ni muhimu kuwahi Hospitali