Takriban watu 200 nchini Haiti waliuawa katika ghasia za kikatili za wikendi zilizoripotiwa kupangwa dhidi ya wanaoshukiwa kuwa wachawi,huku serikali siku ya Jumatatu ikilaani mauaji ya “ukatili usiovumilika.”
Mauaji katika mji mkuu wa Port-au-Prince yalisimamiwa na kiongozi wa genge mwenye nguvu aliyeamini kwamba ugonjwa wa mwanawe ulisababishwa na wafuasi wa imani hiyo, kulingana na shirika la kiraia la Kamati ya Amani na Maendeleo (CPD).
Mtandao wa Kitaifa wa Kutetea Haki za Kibinadamu (RNDDH) ulisema kiongozi wa genge la eneo hilo aliwalenga watu hao baada ya mtoto wake kuugua na kufariki dunia.
Inasemekana kwamba kiongozi huyo wa genge aliwasiliana na kasisi mmoja ambaye aliwalaumu wazee wa eneo hilo wanaofanya “uchawi” na kusababisha ugonjwa wa ajabu wa mvulana huyo.
“Aliamua kuwaadhibu kwa ukatili wazee wote na waganga ambao, kwa mawazo yake, wangeweza kumtumia mwanawe uchawi mbaya,” taarifa kutoka kwenye kikundi chenye makao yake Haiti ilisema
Umoja wa Mataifa ulisema idadi ya watu waliouawa nchini Haiti kufikia sasa mwaka huu katika ongezeko la ghasia za magenge imefikia “kiasi cha watu 5,000”.
Ilikuwa ni kitendo cha hivi punde zaidi cha unyanyasaji uliokithiri wa magenge yenye nguvu ambayo yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu katika nchi maskini ya Karibea iliyozama kwa miongo kadhaa katika ukosefu wa utulivu wa kisiasa, majanga ya asili na matatizo mengine.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilaani ghasia hizo “za kutisha”, ambazo msemaji wake alisema zilisababisha vifo vya takriban watu 184 wakiwemo wazee 127 wanaume na wanawake.
Kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, zaidi ya watu 700,000 – nusu yao watoto – ni wakimbizi wa ndani nchini kote.
Washiriki wa magenge mara nyingi hutumia unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa magenge, ili kuleta hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.