Rais wa Kenya, William Ruto ametangaza kuwa Serikali yake imetuma ombi rasmi la kuandaa Tuzo za Grammy na tayari imelipa kiasi cha shilingi za Kenya milioni 500 (sawa na bilion 10 za Kitanzania) kwa ajili ya maandalizi hayo, akizungumza katika Ukumbi wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) wakati wa maadhimisho ya miaka miwili ya utawala wake Rais Ruto alieleza dhamira ya Serikali yake kukuza sekta ya ubunifu Nchini na kuifanya Kenya kuwa kitovu cha burudani Duniani.
Aidha Rais Ruto alibainisha kuwa ushirikiano wa Kenya na Grammy Global Ventures ulioanzishwa Aprili mwaka huu unalenga kuimarisha ushiriki wa Kenya katika tasnia ya ubunifu ya kimataifa huku akisisitiza umuhimu wa kuingiza sanaa za maonyesho katika mitaala ya elimu Nchini na kuanzisha mafunzo maalum kwa Waelimishaji wa sanaa.
Kwa upande wake Dennis Itumbi Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uchumi wa Ubunifu alifichua kuwa Serikali pia inawania nafasi ya kuwa Mwenyeji wa Kongamano la Uchumi wa Ubunifu Duniani mwaka 2027 hatua itakayoiweka Kenya katika ramani ya kimataifa pia Itumbi alieleza kuwa Mwakilishi wa Grammy Awards atakutana na Rais Ruto wiki hii kwa mazungumzo zaidi kuhusu mradi huo.
Rais Ruto alisisitiza kuwa malipo ya kiasi hicho cha fedha tayari yamefanyika akionyesha imani kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa safari ya mafanikio kwa sekta ya ubunifu nchini Kenya. “Tayari tumeshalipa shilingi milioni 500 na nina hakika kuwa Mwakilishi wa Grammys aliyepo hapa ataidhinisha kuwa tuko kwenye njia sahihi,” alisema Rais Ruto.