Zaidi ya wadau 900 wa sekta ya misitu na mazingira wamekutana jijini Arusha kwenye Kongamano la Tatu la Kimataifa la Utafiti wa Kisayansi wa Misitu, linaloandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI). Lengo kuu la kongamano hilo ni kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu za kuhifadhi mazingira kupitia misitu, huku changamoto kubwa ikiwa ni ukataji holela wa miti unaosababisha kupotea kwa hekta laki nne za misitu kila mwaka.
Mgeni rasmi wa kongamano hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dastan Kitandura, amesema tafiti zinazofanywa na TAFORI zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya misitu na nyuki, huku zikisaidia kuongeza mapato ya taifa na kutoa ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Bw. Revocatus Mushumbusi, ameweka wazi kuwa lengo la kukutanisha wataalamu wa misitu na wafugaji nyuki ni kujadili changamoto za usimamizi wa maliasili, ufugaji nyuki endelevu, na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Lucy Mahenga, ameongeza kuwa utunzaji wa misitu ni muhimu kwa kuhakikisha upatikanaji wa vyanzo vya maji na kusaidia kunyonya hewa ya ukaa inayozalishwa kutokana na shughuli za viwanda duniani.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAFORI, Profesa Veridiana Masanja, ameibua changamoto zinazokumba sekta hiyo, ikiwemo ukosefu wa watafiti wa kutosha, upungufu wa teknolojia na vifaa, miundombinu chakavu ya maabara, pamoja na uhaba wa mafundi wenye ujuzi.
Kongamano hilo limebainisha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kisekta ili kuhakikisha usimamizi endelevu wa misitu na kuendeleza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.