Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol ametetea uamuzi wake wa mshtuko wa kutangaza sheria ya kijeshi wiki iliyopita, akisema alifanya hivyo ili kulinda demokrasia ya nchi hiyo.
Katika hotuba ya mshangao iliyotangazwa na televisheni siku ya Alhamisi, alisema jaribio hilo lilikuwa uamuzi wa kisheria wa “kuzuia kuporomoka” kwa demokrasia na kukabiliana na “udikteta wa bunge” wa upinzani.
Yoon amependekeza kuwa hatajiuzulu kabla ya kura ya pili ya kumshtaki bungeni siku ya Jumamosi.
“Nitasimama kidete iwapo nitashtakiwa au kuchunguzwa,” alisema. “Nitapigana hadi mwisho”.
Rais na washirika wake wanakabiliwa na uchunguzi kuhusu mashtaka ya uasi, na yeye na kadhaa wao wamepigwa marufuku kuondoka Korea Kusini.
Siku ya Alhamisi, bunge linaloongozwa na upinzani lilipiga kura ya kuwashtaki mkuu wa polisi Cho Ji-ho na waziri wa sheria Park Sung-jae.
Maafisa hao wawili wamesimamishwa kazi mara moja.
Tofauti na hoja za kuwashtaki marais, ambazo zinahitaji kura 200 katika Bunge la Kitaifa lenye wabunge 300 kupitishwa, viongozi wengine wanaweza kushtakiwa kwa kura 150.
Katika hotuba yake, ya kwanza tangu aombe msamaha mwishoni mwa juma, Yoon alikanusha kuwa amri yake ya sheria ya kijeshi ilikuwa kitendo cha uasi, akidai kuwa wapinzani wake wa kisiasa walikuwa wakitengeneza “uchochezi wa uwongo” ili kumwangusha.