Rais wa Kenya William Ruto ameongoza taifa katika maadhimisho ya Siku Kuu ya Jamuhuri
Kama ilivyo ada Jeshi la Kenya liliandaa gwaride maalum kwa heshima ya amiri jeshi mkuu wa vikozi vya Ulinzi na Usalama nchini Kenya.
Rais Ruto alikagua gwaride linalofahamika kama Trooping of the colour baada ya wimbo wa taifa kupigwa uwanjani.
Wanajeshi wasiopungua chini ya 180 kutoka vitengo vitatu vya Jeshi la ardhini, angani na majini walifanya maoyesho kadhaa uwanjani wakiongozwa na bendi ya KDF, wenye kuvalia kofia zilizotengezwa kwa ngozi ya tumbili anayefahamika kama COLOBUS MONKEY mwenye manyoya ya rangi nyeusi na nyeupe.
Trooping of the colour ni kuzinduliwa kwa kikosi kipya cha kijeshi ambacho kinapokezwa bendera yake rasmi kwa pamoja na ile ya kitaifa yenye nembo la kikosi hicho juu yake.
Leo ilikuwa zamu ya jeshi la angani ambayo inazindua kikosi kipya kitakachokuwa na makao yake katika mji wa Wajir, uliopo kaskazini Mashariki mwa Kenya, katika kaunti ambayo inapakana na taifa jirani la Somalia.