Askofu Mkuu wa York, Stephen Cottrell anakabiliwa na wito wa kujiuzulu kwa kushindwa kushughulikia kesi ya unyanyasaji wa kingono, siku chache kabla ya kuchukua mamlaka ya muda ya Kanisa la England.
Katika taarifa yake ya kibinafsi Jumatatu, Cottrell alisema hana sababu za kisheria za kuchukua hatua dhidi ya David Tudor hadi 2019, wakati madai mapya yalitolewa dhidi ya kasisi huyo.
Kauli yake ilifuatia uchunguzi wa BBC uliodai kuwa Cottrell alipokuwa askofu wa Chelmsford alimruhusu Tudor kusalia wadhifa huo licha ya kujua kwamba Kanisa la Uingereza lilikuwa limempiga marufuku kuwa peke yake na watoto na alikuwa amelipa fidia ya £10,000 kwa mwathiriwa wa unyanyasaji wa kingono.
Mwanamke aliyepokea fidia hiyo aliambia BBC kuwa alihisi kama Cottrell “amenitemea usoni” kwa kukosa kuchukua hatua alipoambiwa kuhusu malipo hayo.
Rt Rev Helen-Ann Hartley, askofu wa Newcastle, alisema Cottrell anapaswa kusimama. “Askofu mkuu mmoja amejiuzulu kwa kushindwa kulinda, na sasa askofu mkuu aliyesalia ana jambo zito sana ambalo linatilia shaka uwezo wake wa kuongoza mabadiliko ya haraka yanayohitajika,” aliambia BBC Radio 4.
Kufuatia uchunguzi huo, Tudor alipigwa marufuku kutoka wizarani na kufukuzwa kazi miezi miwili iliyopita, baada ya kukiri madai ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto yanayohusiana na wasichana wawili katika miaka ya 1980.
Kufikia wakati huo alikuwa kasisi kwa miaka 46, huko London, Surrey na Essex.
Cottrell alisema “anasikitika sana kwamba hatukuweza kuchukua hatua mapema”.