Wanaume wawili kutoka Rochester, Marekani, wamefariki dunia baada ya kuambukizwa Ugonjwa wa nadra wenye Sumu kuvu unaoshambulia mapafu, baada ya kutumia Kinyesi cha Popo kama Mbolea ya kukuza Bangi.
Mmoja wa Wanaume hao mwenye umri wa miaka 59, alinunua kinyesi cha Popo mtandaoni huku mwingine mwenye umri wa miaka 64, akipanga kutumia kinyesi kutoka kwenye dari ya Nyumba yake iliyojaa Popo ambapo wote wawili walipatwa na dalili kama homa, kikohozi cha muda mrefu, kupungua uzito, sumu kwenye damu na mwishowe kushindwa kupumua.
Licha ya matibabu ya haraka ikiwemo tiba ya Sumu kuvu wote walifariki dunia ambaoo kupitia Ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la Open Forum Infectious Diseases ilibainisha kuwa Ugonjwa huo unajulikana kitaalam kama histoplasmosis ambao husababishwa na Sumu kuvu hatari inayopatikana kwenye vinyesi vya Popo.
Kutokana na ongezeko la kilimo cha Bangi kufuatia hatua za kuhalalisha matumizi yake, kinyesi cha Popo kimekuwa kikipendekezwa kama Mbolea asilia yenye uwezo wa kuongeza mazao jambo linalovutia Watu wengi bila kufahamu hatari zake.
Aidha Taasisi za afya zimeshauriwa kuongeza kampeni za uhamasishaji ili kuzuia vifo vya aina hii huku Wataalamu wakisisitiza kuwa Mbolea za kibiashara zinazotumia kinyesi cha Popo zinapaswa kufanyiwa vipimo vya Sumu kuvu hatari kabla ya kuuzwa sokoni.