WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi ya dharura iliyo chini ya wizara hiyo.
Waziri Ulega ametoa maagizo hayo kwenye mkutano wake na Menejimenti na Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini uliofanyika mjini Dodoma ambapo amewaambia miradi ya dharura inapaswa kushughulikiwa kidharura.
“Fanyeni kazi kwa kasi tena usiku na mchana hususan kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa,” amesema Ulega.
Ulega amewaambia mameneja hao kuwa wanatakiwa waende kwa spidi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na serikali kwa sababu kuna mvua zinakuja na zinaweza kufanya maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.
Ulega amesema barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua za masika zilizochanganyika na zile za El Niño zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka.
Mkutano wa Dodoma ulikuwa ni wa kwanza kwa Ulega kukutana na viongozi wa TANROADS tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais Dk Samia Suluhu Hassan mwezi huu.