Mwanamume mmoja amekamatwa huko New York kuhusiana na kifo cha mwanamke aliyechomwa moto kwenye treni ya chini ya ardhi huko Brooklyn.
Kamishna wa polisi Jessica Tisch alielezea tukio hilo la Jumapili kama “moja ya uhalifu mkubwa ambao mtu anaweza kufanya dhidi ya binadamu mwingine”.
Alisema mwanamke huyo alikuwa kwenye treni ya F kuelekea Brooklyn alipofikiwa na mwanamume aliyetumia njiti kuwasha mavazi yake moto.
Mwathiriwa alifariki katika eneo la tukio, alisema, na kuongeza kuwa mshukiwa alikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa kundi la wanafunzi wa shule ya sekondari alipokuwa kwenye treni ya chini ya ardhi baadaye Jumapili.
Polisi walisema mwanamke huyo, ambaye hajatajwa jina, alikuwa kwenye treni ya chini ya ardhi katika kituo cha Coney Island-Stillwell Avenue huko Brooklyn yapata saa 07:30 saa za huko (12:30 GMT) wakati mwanamume alipomwendea na kufanya tukio hilo
Hakukuwa na mwingiliano wowote kabla ya shambulio hilo, polisi walisema, na kuongeza kuwa hawakuamini kuwa watu hao wawili walijuana.
Polisi bado wanafanya kazi ya kubaini mwathiriwa na sababu za shambulio hilo