Idadi ya vifo vilivyotokana na kimbunga Chido nchini Msumbiji imefikia watu 94. Idadi hiyo ni kwa mujibu wa shirika la kukabiliana na majanga nchini humo.
Kimbunga Chido kiliipiga pwani ya Msumbiji yapata wiki moja iliyopita, japo eneo lililoathiriwa zaidi na kimbunga hicho ni visiwa vya Mayotte.
Inaarifiwa kuwa, kimbunga hicho kimefanya uharibifu mkubwa katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado. Takriban watu 620,00 wameathirika na kimbunga hicho nchini Msumbiji, wakati 500,000 kati ya hao wakiishi Cabo Delgado.
Wataalamu wanasema kimbunga Chido kimekuwa na nguvu zaidi kutokana na athari ya mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Jimbo la Cabo Delgado hukumbwa mara kwa mara na vimbunga vya tropiki lakini pia jimbo hilo linakabiliwa na vurugu zinazotokana na uasi wa muda mrefu.