Zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Korea Kaskazini waliuawa au kujeruhiwa katika mapigano dhidi ya vikosi vya Ukraine, kamati ya wakuu wa majeshi ya Korea Kusini (JCS) imesema leo Jumatatu (Desemba 23).
“Tunakadiria kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini, ambao hivi majuzi walishiriki katika mapambano dhidi ya vikosi vya Ukraine, walipoteza karibu wanajeshi 1,100,” JCS imesema katika taarifa.
Makao makuu ya mjeshi ya Korea Kusini pia yameshuhudia maandalizi ambayo yanaifanya kuamini kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kutuma wanajeshi wengine nchini Urusi, kama nyongeza au kuchukuwa nafasi ya wale ambao tayari wanapigana.
Taarifa za ujasusi zilizokusanywa na Korea Kusini zinaonyesha kwamba Korea Kaskazini “inatengeneza na kutoa ndege zisizo na rubani zenye kulipuka” kwa Urusi, ambayo pia inatoa”silaha za kurusha roketi “, JCS inabainisha.
Jeshi la Korea Kusini linabaini kwamba Korea Kaskazini inatafuta kurekebisha uwezo wake wa vita vya kawaida kwa usaidizi wa Urusi, kulingana na uzoefu wake wa mapigano dhidi ya vikosi vya Ukraine.
“Hii inaweza kusababisha ongezeko la tishio la kijeshi la Kaskazini dhidi yetu,” imesema JCS.
Maelfu kadhaa ya wanajeshi wa Korea Kaskazini wametumwa Urusi katika wiki za hivi karibuni kusaidia jeshi la Urusi, kulingana na nchi za Magharibi.