Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kiwango cha tishio kinaongezeka duniani kote, lakini hakuna haja ya kuwatisha watu kuhusu Vita vya Tatu vya Dunia.
Wakati wa mahojiano yaliyochapishwa na mwandishi wa habari wa TV 1, Pavel Zarubin siku ya Jumapili, Putin aliulizwa ikiwa ushiriki mkubwa wa Marekani katika mzozo kati ya Russia na Ukraine unamaanisha kwamba Vita vya Tatu vya Dunia tayari vimeanza.
Katika kujibu, Putin amesema: “Unajua haipaswi kuwatisha watu.” Hata hivyo, aliongeza kwamba “kuna hatari nyingi, na zinaendelea kuongezeka.”
Kuhusu mipango ya utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden, kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya silaha zinazopelekwa Ukraine katika wiki zake za mwisho madarakani, Putin amesema: “Tunaona wanachofanya wapinzani wetu wa sasa.
Wanazidisha taharuki.”
Aidha amesema: “Ikiwa wanataka sana taharuki, ikiwa maisha yao ni mabaya sana, wacha wazidishe basi.” Putin amesisitiza kwamba Russia “daima itajibu changamoto yoyote” kutoka madola ya Magharibi.
Rais wa Russia ameendelea kusema kuwa: “Wakati wapinzani wetu wa sasa – na labda washirika watarajiwa – hatimaye watasikia, kuelewa na kutambua hili, inaonekana kwangu kwamba wakati huo watatambua kwamba kinachohitajika ni kutafuta maelewano.”
Putin amesema Moscow iko tayari kujaribu kujenga tena uhusiano na Marekani na washirika wake, lakini inapaswa kutokea bila kudhuru masilahi ya Russia.