Qatar ilifungua tena ubalozi wake mjini Damascus siku ya Jumamosi, miaka 13 baada ya kuufunga wakati wa hatua za mwanzo za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Hatua hii inajiri huku serikali za kigeni zikianza kuanzisha tena uhusiano na uongozi mpya wa nchi.
Mwandishi wa habari kutoka shirika moja la habari alishuhudia bendera ya Qatar ikipandishwa juu ya ubalozi huo, na kuifanya Qatar kuwa nchi ya pili, baada ya Uturuki, kufungua rasmi ujumbe wake wa kidiplomasia tangu waasi wanaoongozwa na Waislam walipompindua Rais Bashar al-Assad mapema mwezi huu.
Tofauti na mataifa mengine ya Kiarabu, Qatar, ambayo iliunga mkono makundi ya upinzani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ilijizuia kumrekebisha Assad kabla ya kuondolewa kwake.
Mapema siku ya Jumamosi, wafanyikazi walisafisha eneo karibu na ubalozi, wakaondoa maandishi, na kufagia barabara. Mfanyikazi mmoja aliweka bendera ya Qatar chini ya nguzo kabla ya kupandishwa.
Doha ilikuwa imetuma wajumbe wa kidiplomasia kwenda Damascus siku zilizopita kukutana na serikali ya mpito. Ujumbe huo ulionyesha “dhamira kamili ya Qatar ya kusaidia watu wa Syria,” kulingana na mwanadiplomasia wa Qatar akizungumza na AFP.