Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana amemuapisha na kumvika cheo kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Dkt Elirehema Joshua Dorie na kumwagiza kuhakikisha anapanua wigo wa watalii Ngorongoro ili kuvutia watalii zaidi, kuimarisha miundo mbinu ya utalii pamoja na kuimarisha mahusiano ya watumishi na wadau mbalimbali ndani na nje ya mamlaka hiyo.
Aidha amempongeza Dkt Dorie kwa kuwa Katika kipindi kifupi cha uongozi wake ameweza kuonyesha uwezo mzuri wa usimamizi wa mapato, matumizi ya mifumo ya tehama, kuimarisha mahusiano ya kikazi baina ya watumishi na kutengeneza mifumo inayo weza kurahisisha kazi na usimamizi wa haki za watumishi.
Akitoa salamu za bodi ya wakurugenzi NCAA Jenerali Venance mabeyo mstaafu akampongeza Dkt Dorie kwa uapisho huku Akieleza licha ya mafanikio mbalimbali waliyopata na wanavyoendelea kupata bado wana matarajio makubwa kwake baada ya uapisho huo.
Nae Dkt. Elirehema Joshua Dorie Kamishna wa uhifadhi hifadhi ya taifa ya Ngorongoro akamshukuru raisi kwa kumpa nafasi hiyo na kuahidi kuongoza kwa kujituma, kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kufikia malengo ya wizara na serikali kwa ujumla
Aidha ameongeza kuwa dhamira yake kuu katika uongozi wake ni kuhakikisha anasimamia na kulinda uhifadhi endelevu, kukuza zaidi utalii wa kimkakati kwa kuimarisha miundombinu ili kuhakikisha uhifadhi unakuwa chanzo kikuu cha mapato ya taifa pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kukuza mahusiano baina ya hifadhi na jamii.