Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule pindi msimu mpya wa masomo unapoanza Januari 13, 2025 ambapo mkoa wa Katavi una jumla ya wanafunzi 13,887 watakaojiunga na shule za sekondari.
Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi ametoa rai hiyo wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake leo.
Bi. Mrindoko amesema kuwa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hao tayari yamekamilika ambapo mahitaji yalikuwa ni kuwa na vyumba 283 lakini mpaka sasa vyumba vilivyopo ni 311 sawa na ongezeko la vyumba vya madarasa 28 kwa mkoa mzima.
“Hatuna wasiwasi wa namna wanafunzi hawa watakavyoanza shule ifikapo Januari 13, mwaka ujao” alisema.
Aidha kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza mkuu huyo wa mkoa wa Katavi alisema mpaka sasa uandikishaji wa wanafunzi umefikia asilimia 34.2 hali ambayo hairidhishi na kuwasisitiza wazazi na walezi kuendelea kuwaandikisha watoto.
Amewataka viongozi wa serikali za mitaa kupita katika nyumba za mitaa yao, vijiji na vitongoji kufanya ufuatiliaji na watoto wanaostahili kuanza shule ili waandikishwe.
“Watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka minne waandikishwe shule” alisisitiza.
Pia Bi. Mrindoko ameagiza watoto wote wa shule za sekondari na msingi wawe wanapata chakula cha mchana.
“Tumetoa ruhusa kwa shule kufanya vikao na wazazi kukubaliana namna ya kuchangia chakula cha wanafunzi, hivyo nitoe rai kwa wazazi wote kwamba kile watakachokubaliana kuchanga basi wasisite kuchanga ili watoto wetu wapate chakula shuleni” alisisitiza Bi. Mrindoko.