Zaidi ya wananchi 20,000, wanatarajiwa kupatiwa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa yasiyoambukizwa, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo, presha, na kisukari, katika maeneo mbalimbali nchini hadi kufikia mwaka 2025.
Huduma hiyo inatekelezwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mpango wa ‘Dk. Samia Suluhu Tiba Mkoba’ unaowawezesha madaktari bingwa wa taasisi hiyo kutoa huduma bure katika mikoa mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge, alisema kuwa hadi sasa, wananchi 18,000 kutoka mikoa 17 wamepatiwa huduma hiyo, ikiwa ni pamoja na upimaji na matibabu kwa wale waliobainika na magonjwa hayo.
“Kwa kuanzisha huduma ya Dk. Samia Suluhu Tiba Mkoba, Januari mwaka jana, tumeweza kuwafikia wananchi wengi na kusaidia kuimarisha afya zao, mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa,” alisema Dk. Kisenge.
Alisema wasanii kutoka sekta ya uigizaji, uimbaji, na uchekeshaji pia wamejitokeza kupima afya zao, ili kujua hali zao na kupata matibabu mapema.