Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema wanajeshi zaidi ya 3,000 wa Korea Kaskazini wameuawa au kujeruhiwa katika mapigano eneo la Urusi la Kursk.
Zelenskyy alisema katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kuwa idadi hiyo iliripotiwa na Kamanda Mkuu wa jeshi la Ukraine Oleksandr Syrskyi.
Ukraine inafanya mashambulizi ya kuvuka mpaka katika eneo la Kursk. Wanajeshi wapatao 11,000 wa Korea Kaskazini wamesemekana kupelekwa katika eneo hilo sambamba na wale wa Urusi.
Zelenskyy ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua ya kimataifa, akiandika kuwa “kwa bahati mbaya, dunia haifanyi chochote kukabiliana na ushirikiano wa kihalifu kati ya Urusi na Korea Kaskazini.”
Idadi ya wanajeshi waliouawa wa Korea Kaskazini waliotajwa na Zelenskyy inazidi kwa mbali ile iliyotolewa na idara ya ujasusi ya Korea Kusini wiki iliyopita.