Polisi nchini Japani wanasema kundi la wadukuzi wa Korea Kaskazini huenda walitumia ujumbe wa ofa ya kazi kuiba mali kutoka kwa kampuni ya kubadilisha sarafu za mtandaoni ya DMM Bitcoin mwezi Mei mwaka huu.
Wizi huo uliigharimu kampuni hiyo sarafu za bitcon zenye thamani ya takriban dola za Marekani milioni 308 wakati wa udukuzi huo.
Awali, kampuni hiyo ilisema inafunga biashara zake baada kukabidhi akaunti na mali za wateja wake kwa kampuni nyingine ya kubadilisha fedha.
Idara ya Taifa ya Polisi ya Japani na Idara ya Polisi ya Jiji la Tokyo zilitangaza leo Jumanne kuwa TraderTraitor ilihusika katika wizi huo.
TraderTraitor ni tawi la kundi la udukuzi la Lazarus linaloaminika kuwa kundi lililo chini ya mamlaka za Korea Kaskazini.
Polisi wamesema mfanyakazi wa kampuni inayosimamia sarafu za mtandaoni za DMM Bitcoin alipokea ujumbe kwenye mitandao ya kijamii mwezi Machi mwaka huu kutoka kwa mtu mmoja aliyedai kuwa mwajiri wa wafanyakazi kutoka kampuni nyingine.
Ujumbe huo unaaminika kuweka virusi vya kompyuta ulipobonyezwa na kuliruhusu kundi hilo kuiba taarifa ya kufungua kompyuta hiyo na kuandika upya kiasi cha miamala na wanufaikaji.
Polisi wanasema akaunti hiyo ya mitandao ya jamii iliyotuma ujumbe huo na seva iliyounganishwa nayo zilikuwa na uhusiano na Korea Kaskazini.