Mahakama ya Kikatiba nchini Korea Kusini imetangaza kwamba itafanya maandalizi ya awali ya kusikiliza kesi ya kumwondoa madarakani Rais Yoon Suk-yeol Ijumaa wiki hii kama ilivyopangwa.
Tangazo hilo limekuja kufuatia ripoti za vyombo vya habari nchini humo kuwa huenda maandalizi ya kusikiliza kesi hiyo yakacheleweshwa kwa sababu Yoon amekataa kupokea nyaraka za mahakama zinazomtaka kuhudhuria kesi hiyo.
Jana Jumatatu, mahakama hiyo ilisema itachukuliwa kuwa Yoon amepatiwa nyaraka zinazohitajika kuhusiana na kesi hiyo.
Hata hivyo, mahakama hiyo haikueleza namna itakavyoitikia ikiwa Yoon hatahudhuria kusikilizwa kwa kesi hiyo, ikisema itakuwa ni juu ya majaji wa mahakama hiyo kufanya uamuzi.
Wakati huo huo, timu ya mamlaka ya pamoja ya uchunguzi, inayojumuisha polisi, ilituma wito wa pili wa kufika shaurini kwa mahojiano katika ofisi ya Yoon Jumatano iliyopita. Lakini timu hiyo inasema haiwezi kuthibitisha ikiwa ofisi hiyo ilipokea hati hizo.
Vyombo vya habari nchini Korea Kusini vimemnukuu mwanasheria aliye karibu na Yoon akisema kwamba rais huyo ameelezea utayari wa kutoa kipaumbele kwa taratibu za kesi ya kumwondoa madarakani, badala ya kuitikia uchunguzi huo kuhusiana na uasi na matumizi mabaya ya madaraka.