Bodi ya michezo ya kubahatisha (GBT) yazindua kampeni Fichua, Tukomeshe Mashine Haramu za Dubwi, kamata kamata kufanyika nchi nzima
Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kwa kushirikiana na wenyeviti wa serikali za mitaa wa mkoa wa Dar es Salaam wamezindua kampeni maalum ya kutokomeza uchezaji wa mashine maarufu za dubwi kinyume na utaratibu.
Kampeni hiyo iliyopewa jina la Fichua, Tukomeshe Mashine Haramu ilizunduliwa jijini jana ikienda sambamba na semina kwa washiriki ili kujua mashine ‘feki’ zinazotumika na kuipotezea taifa fedha.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw James Mbalwe alisema kuwa wamepokea malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na kuenea kwa mshine za dubwi na kutimika kwa watoto chini ya miaka 18 ambapo ni kinyume na sheria.
Alisema kuwa, mbali ya kuwatumika kwa watoto wadogo, pia mashine hizo zimewekwa kwenye nyumba za kuishi tofauti na baa au sehemu za burudani ambapo ni kinyume cha sheria.
“Pia wapo waliowahusisha watoto chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha, jambo ambalo ni kinyume cha kisheria ya nchi, ” alisema Bw Mbalwe.
Alisema kuwa pamoja na kwamba mchezo wa dubwi upo kisheria, wapo wachezeshaji wanaouendesha kinyume cha sheria bila leseni na vile vile kutumia mashine zilizoingia nchini kwa njia ya ‘panya’.
“Hawa ndiyo wanaosababisha sintofahamu hii huko mitaa, sasa kupitia kampeni hii, tutawasaka na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisisitiza.