Wanawake na Wafanyakazi wa mkoa wa Dar es salaam kupitia wilaya ya Ubungo wametakiwa kuendelea kujiunga kwenye Vyama mbalimbali vyenye kutoa fursa mbalimbali ikiwepo kupata elimu namna ya kujikomboa na kuweza kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii.
Kauli hiyo imesemwa leo na Mwenyekiti wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi wilaya ya Ubungo na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi mkoa wa Dar es Salaam Hidaya Njaidi wakati wa kongamano la Usiku wa Mwanamke ambapo Wanawake Wafanyabiashara na Wafanyakazi wamekutana na kujadiliana namna ya kusonga mbele kiuchumi.
“Ubungo tuna wanachama wengi sana ambao wamejiunga na tunaamini kuna wengine wataendelea kujiunga nitoe wito kwenu wanawake wafanyabiashara na Wafanyakazi muendelee kujiunga kwenye vyama venye tija kwa lengo la kutatua changamoto zenu za kiuchumi na kijamii na kuondokana na mikopo isiyoyalazima” Amesema Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Vijana Right of Success, Zena Mlokosi amesema lengo kuu ni kuendeleza Umoja kwa Wanawake Wafanyabiashara na Wafanyakazi kwa kusaidia waliokwama kwani Wanawake zaidi ya 250 tumekutana na kufundishana namna ya kujikomboa kiuchumi kupitia njia ya ujasiriamali na uwekezaji.