Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) katika Wilaya ya Wenchi magharibi Nchini Ghana limewatunuku Wasichana 20 wenye umri kati ya miaka 13 hadi 16 kwa kulinda usichana wao ambapo tukio hilo lilifanyika wakati wa ibada ya shukrani ya sabato ya kwanza ya mwaka 2025, ambapo kila Msichana alipewa zawadi ya fedha kwa ajili ya mahitaji yao.
Mratibu wa Shirika la Young Adventist Women Ministries, Nana Amponsah Poku aliwasifu Wasichana hao kwa maamuzi yao ya busara na kuwataka waendelee kujiheshimu hadi kufikia ndoa pia alisisitiza umuhimu wa mila za kitamaduni kama sherehe za utu uzima katika kukuza maadili mema na kupunguza changamoto kama mimba za utotoni.
Aidha Mchungaji Msaidizi wa Wilaya hiyo, Andrews Dua Bour Kyere naye aliwapongeza Wasichana hao kwa mfano mzuri waliouonyesha na kuwataka waendelee kuwa safi kiroho huku wakijikita zaidi katika masomo yao.
Wasichana waliotunukiwa walionyesha furaha yao na kulitaja Kanisa kama nguzo muhimu katika malezi yao ya kiroho na kijamii pia waliwashukuru viongozi wa kanisa kwa msaada wao katika kukuza maadili bora.