Tembo amemuua mwanamke mmoja raia wa Uhispania alipokuwa akimwogesha mnyama huyo katika kituo cha tembo nchini Thailand, wamesema polisi wa eneo hilo.
Blanca Ojanguren García, 22, alikuwa akiosha tembo katika Kituo cha Kutunzia Tembo cha Koh Yao, siku ya Ijumaa iliyopita alipouawa kwa kupigwa na pembe za tembo.
Wataalamu wa tembo waliliambia gazeti la lugha ya Kihispania, Clarín kwamba huenda tembo huyo alikuwa na hofu baada kulazimika kutangamana na watalii nje ya makazi yake ya asili.
García, mwanafunzi wa sheria na mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Navarra nchini Uhispania, alikuwa akiishi Taiwan kama sehemu ya mpango wa kubadilishana wanafunzi.
Alikuwa katika matembezi nchini Thailand akiwa na mpenzi wake, ambaye alishuhudia shambulio hilo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania, Jose Manuel Albares, amesema ubalozi mdogo wa Uhispania huko Bangkok unaisaidia familia ya García.