Katika kuukaribisha mwaka mpya 2025, Benki ya CRDB imezindua mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote. Mikopo hiyo inayoitwa Ada Fasta ni mwendelezo wa juhudi za Benki ya CRDB kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kifedha wanakokabiliana nazo.
.
Akizindua mikopo hiyo inayotolewa kupitia Programu ya SimBanking, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema kila mzazi au mlezi mwenye uhitaji anaweza kupata mkopo huo ili kumruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo kulingana na ratiba ya muhula husika.
.
“Mteja anaweza kukopa mpaka shilingi milioni 3 ambazo atazirudisha ndani ya miezi sita. Riba ya mkopo huu ni asilimia 13 tu mwaka, gharama ndogo zaidi ukilinganisha riba iliyopo sokoni. Nawakaribisha wazazi wote kuitumia fursa hii kuhakikisha watoto wetu wanasoma bila tatizo lolote la ada,” amesema Nshekanabo.
Mkurugenzi huyo amesema wameizindua huduma hiyo kipindi hiki wakitambua kuwa Januari ni mwezi wenye changamoto nyingi za kifedha zinazotokana na mahitaji makubwa yanayokuwepo ikiwamo ada za wanafunzi, kodi ya nyumba na mahitaji mengine muhimu hasa baada ya kila mtu kuwa ametumia kiasi kikubwa cha fedha kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
.
Ikiwa Benki inayomsikiliza mteja na kumweka mbele katika mikakati ya biashara, amesema wakati wote wanabuni huduma na bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wateja na Januari hii wamekuja na jambo jipya mahususi kwa kila mzazi au mlezi wa mwanafunzi nchini.
.
Zaidi ya muongo mmoja Benki ya CRDB ilizindua nakuutambulisha Mfumo wa Makusanyo ya Ada Shuleni yaani School Fees Management System ambao mpaka sasa unatumiwa na zaidi ya shule 1,000 nchini kote ambazo sasa wanafunzi wake watanufaika na mikopo hii iliyozinduliwa.
“Hii ni fursa kwa shule zote binafsi nchini kujiunga na mfumo huu wa makusanyo ya ada ii kutoa fursa kwa wazazi kukopa ada wakati wowote watakapohitaji ili watoto waendelee na masomo yao. Wazazi wote waliopo kwenye shule zinazoutumia mfumo huu wawe ni wateja wetu ama la, wanayo fursa ya kunufaika na mikopo hii,” amesema Nshekanabo.
.
Mzazi au mlezi atakayeomba mkopo huu, amesema atapata fedha husika zitakazoingizwa kwenye akaunti ya shule moja kwa moja na yeye kupata risiti ya uthibitisho kwamba amelipa ada inayotakiwa kwa ajili ya mtoto wake.
.
Kwa kuwawezesha wazazi na walezi kulipa ada kwa wakati, Nshekanabo amesema wana imani watakuwa wamesaidia kuboresha elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo yao bila vikwazo huku shule zikiweza kujiendesha na kutoa maarifa bora yanayohitajika kwa watoto wa Kitanzania.
Kwa mzazi au mlezi ambaye ameajiriwa na mshahara wake unapitia Benki ya CRDB, anaweza kupata mkopo wa ada kwa kuingia kwenye Programu ya SimBanking kisha akabofya sehemu ya mikopo ambako atatakiwa kuingiza ‘control number’ aliyotumiwa na shule kwa ajili ya malipo ya ada na programu itamwonyesha kiasi cha juu anachoruhusiwa kukopa.
.
Baada ya hapo, mteja atatakiwa kuingiza kiasi anachokitaka na kupendekeza muda anaotaka kulipa deni hilo ndani ya miezi sita ili kukamilisha maombi yake. Akishafanya hivyo, Benki ya CRDB itaingiza fedha zilizoombwa kwenye akaunti ya shule anakosoma mtoto hivyo kumruhusu asome kwa utulivu.
.
Ukiacha faida zilizopo kwa pande zote mbili yaani shule na mzazi au mlezi, mfumo wa makusanyo ya ada wa Benki ya CRDB ni rahisi kuutumia kwani mteja anaweza kulipa ada kupitia SimBanking, CRDB Wakala au kutembelea tawi la Benki ya CRDB.
.
Vilevile, mteja anaweza kulipa ada ya mwanafunzi kupitia M-pesa, Tigopesa, Airtel Money au Halopesa bila kulazimika kupeleka risiti ya malipo shuleni kwani taarifa huwa zinafika huko moja kwa moja. Kwa upande wa shule, faida iliyopo ni kwamba inakusanya ada kwa wakati na kupata taarifa papo hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.
.
Rais wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu nchini (TAPIE), Mahmod Mringo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.