Kesi ya mauaji ya kukusudia ya mtoto Greyson Kanyenye (6), aliyekuwa akiishi Ilazo, jijini Dodoma, inayowakabili washtakiwa Kelvin Joshua (27) ambaye ni dereva bodaboda na Tumaini Msangi (28), bondia, imeahirishwa hadi Januari 27, mwaka huu itakapotajwa tena.
Washtakiwa hao wawili walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Desemba 30, 2024 kwa kosa la kuua kwa kukusudia tukio lilitokea mtaa wa Ilazo jijini Dodoma, Kata ya Ipagala Desemba 25, mwaka jana.
Hakimu Mkazi Daraja la kwanza, Charles Eligy, aliahilisha kesi hiyo jana hadi Januari 27, mwaka huu itakapotajwa tena huku washtakiwa wote wawili wakiendelea kusota mahabusu kutokana na kosa lao kukosa dhamana.
“Shauri hili linaahirishwa hadi Januari 27, mwaka huu litakapotajwa tena na washtakiwa wote wawili mtaendelea kubaki mahabusu kutokana na kosa lenu halina dhamana,” alisisitiza Hakimu Eligy.
Awali, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Patricia Mkina, aliiambia mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea.
“Mheshimiwa hakimu shauri hili lilikuja leo mbele yako kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea hivyo kwa ridhaa yako tunaomba utupangie siku nyingine kwa ajili ya kutajwa tena,” alisema Mkina.
Desemba 30, mwaka jana, Wakili Mkina akisoma hati ya mashtaka, alisema washtakiwa wote wawili walifanya kosa la mauaji ya Greyson Desemba 25, 2024.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mkazi Denis Mpelembwa, alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mauaji.
“Kosa la mauaji halina dhamana hivyo mtarudi mahabusu hadi kesi yenu itakapotajwa tena Januari 13, 2025,” alisema Hakimu Mpelembwa.