RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) uliopangwa kufanyika February 21 hadi 22,mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Januari 14,2025 jijini Dodoma na Waziri wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo ambao umeandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Kahawa la Afrika (IACO) kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika.” .
Bashe amesema mkutano huo utahudhuriwa na Wakuu wa nchi zinazolima Kahawa Barani Afrika, Mawaziri wa Kilimo, Sekta Binafsi, Viongozi wa Taasisi za Kahawa katika nchi zinazolima Kahawa, Wakulima na Wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa Kahawa.
“Mkutano huu utatoa mwongozo wa jinsi ya kushirikiana na Umoja wa Afrika na Mashirika yake, Benki za Maendeleo za Afrika na taasisi nyingine za fedha ili kuunda programu zinazochochea ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia Sekta ya Kahawa.”amesema Mhe.Bashe
Amesema lengo la Tanzania kuomba uwenyeji wa mkutano huo ni pamoja na kutaka kuwaelewesha watanzania juu ya umuhimu wa zao la Kahawai hapa nchini na duniani kote,lakini kushawishi wakulima wajikite katika kilimo hiko.
Bashe amesema kuwa uzalishaji wa zao la Kahawa hapa nchini umeongezeka kutoka tani 34,000 hadi kufikia Tani 85,000 kwa mwaka jana,ambapo alisema hiyo ni hatua kubwa katika kilimo cha zao hilo.
“Serikali iko katika hatua za kuliongezea mnyororo wa thamani wa zao hilo,ndio maana wameandaa mkutano huo ili wadau wa sekta ya Kahawa kuja.kubadilisha mawazo kuhusu zao hilo lakini pia kuona umuhimu wa biashara hiyo dunianie”amesema Bashe .