Waokoaji wa Afrika Kusini wametoa maiti 60 na manusura 82 kutoka kwa mgodi wa dhahabu chini ya ardhi katika siku mbili za operesheni, polisi walisema Jumanne, na kuongeza kuwa walionusurika wote watakabiliwa na mashtaka ya uchimbaji haramu madini na uhamiaji.
Polisi walianza kuzingira mgodi huo mwezi Agosti na kukata chakula na maji kwa miezi kadhaa katika jaribio la kuwalazimisha wachimbaji hao watoke nje ili wakamatwe kama sehemu ya msako dhidi ya uchimbaji haramu.
Mamia zaidi ya wanaume na makumi ya miili zaidi bado imenaswa chini ya ardhi, kulingana na kikundi cha haki za wachimba migodi ambacho kilitoa picha Jumatatu zikionyesha maiti na manusura waliokonda kusalia mifupa kwenye mgodi huo.
Shughuli za uokoaji, zinazohusisha utumiaji wa ngome ya chuma kuwaokoa wanaume na miili kutoka kwenye shimo la mgodi ulio zaidi ya kilomita 2 chini ya ardhi, zitaendelea kwa siku kadhaa, huku polisi wakisema watatoa taarifa za kila siku kuhusu nambari.
Timu ya Reuters katika eneo hilo, yapata kilomita 150 (maili 90) kutoka Johannesburg katika mji wa Stilfontein, iliona waokoaji wakiwa wamembeba mtu mmoja kwenye machela siku ya Jumanne.