Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Touadera, amewasili jijini Moscow kwa mazungumzo yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa nchi yake na Urusi, imethibitisha Kremlin.
Moscow ina uhusiano wa karibu na taifa hilo la Afrika ya kati, ikiwatuma mamia ya wakufuzi wa kijeshi kuusaidia utawala wa Touadera katika vita dhidi ya makundi ya waasi.
Wakati wa ziara yake ya siku tatu, Touadera atakutana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin siku ya Alhamis kuzungumzia kile ambacho Moscow imekitaja kama masuala ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili bila ya kutoa maelezo zaidi.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amekuwa akitoa msaada wa kijeshi wa baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika, nchi yake ikitafuta uungwaji mkono kwenye bara hilo.
Moscow imelenga kuimarisha ushawishi wake barani Afrika katika siku za hivi karibuni, ikitoa msaada wa kijeshi kwa baadhi ya viongozi wa bara hilo.
Jamhuri ya Afrika ya kati, mojawapo ya mataifa maskini zaidi barani Afrika, imekabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika kipindi kirefu.
Mamluki kutoka katika kundi la wapiganaji wa Urusi Wagner, wamekuwa wakiwasaidia wanajeshi katika taifa hilo la Afrika tangu mwaka wa 2018, Moscow pia ikitoa mafunzo kwa maelfu ya wanajeshi hao na mafunzo.