Cuba Jumatano ilianza kuwaachia huru wafungwa waliowekwa jela kufuatia maandamano ya kuipinga serikali ya mwaka 2021, kutokana na makubaliano iliyofikia na utawala wa Biden wiki hii.
Rais wa Marekani Joe Biden anayemaliza muhula wake Jumanne aliiondoa Cuba kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi na kuondoa msururu wa vikwazo vilivyotekelezwa na Donald Trump wakati wa utawala wake wa kwanza, ambavyo vilichangia katika mzozo mbaya wa kiuchumi katika kisiwa hicho kinachoongozwa na utawala wa kikomunisti kwa miongo kadhaa.
Saa chache baada ya tangazo la Marekani, Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alisema Cuba “Itawaachilia “polepole” wafungwa 553 kutoka kwenye magereza yake kufuatia mazungumzo na Vatican.
Katika maandamano ya mwezi Julai mwaka 2021, maandamano makubwa tangu mapinduzi ya Fidel Castro ya 1959, maelfu ya watu waliingia barabarani katika miji kisiwani humo kote, wengi wakiandamana dhidi ya uhaba wa chakula, dawa na umeme, huku visa vya COVID 19 vikiongezeka.
Makundi ya haki za binadamu yanasema takriban watu 1,000 walikamatwa baada ya maandamano hayo.