Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, amesema kuwa uwekezaji mkubwa unaofanyika katika Sekta ya Afya ni juhudi za Serikali za kuboresha huduma za Afya, hatua inayoiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazotoa huduma bora barani Afrika.
Dkt. Jingu aliyasema hayo leo, Januari 16, 2025, wakati akipokea pongezi kutoka kwa taasisi ya Babuu Cancer Foundation kwa mchango wa serikali katika kuboresha sekta ya afya na kuhamasisha mtindo bora wa maisha ndani ya jamii.
Aidha, Dkt. Jingu amesisitiza umuhimu wa jamii kuepuka mitindo ya maisha isiyofaa kwa kuzingatia mlo sahihi na kufanya mazoezi.
Amebainisha kuwa, jukumu la kuwahamasisha wananchi kubadilisha mitindo ya maisha ni kazi ya pamoja kati ya Serikali, Wadau, na wananchi wenyewe.
“Tunapaswa kuendeleza juhudi hizi kwa kushirikiana kuihamasisha jamii kubadili mtindo wa maisha na kuachana na mfumo wa uvivu. Ni muhimu kuhakikisha watu wanazingatia ulaji wa mlo kamili na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara wa Afya,” alisema Dkt. Jingu.
Katika kikao hicho, Cedou Mandingo, maarufu kwa jina la Babu wa Kitaa, alikabidhi cheti cha shukrani kwa Wizara ya Afya kutokana na uwekezaji huo.
Aliongeza kwa kusema kuwa yeye ni miongoni mwa walionufaika na maboresho ya sekta ya afya, kwani ameweza kunusurika na saratani kutokana na huduma bora zinazotolewa.
Katika hatua nyingine Dkt. Jingu pia alihimiza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kama hatua muhimu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila vikwazo. Alisisitiza kuwa bima hiyo itahakikisha usawa na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.