Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kuwa uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa hadi kufikia mwezi Desemba, mwakajana ni jumla ya Megawati 3,091.71 ikilinganishwa na Megawati 2,842.96 zilizokuwepo mwezi septemba, 2024 ikiwa ni ongezeko la Megawati 248.75 sawa na asilimia 8.75.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga Januari 16, 2024 jijini Dodoma, wakati wa kujadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu hali ya uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini kwa kipindi cha kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba, 2024 kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
“Ongezeko hilo lilitokana na kuingia kwa Megawati 235 kutoka katika Mradi wa JNHPP pamoja na mitambo ya Kigoma kuingia kwenye Gridi ya Taifa.” Smesema Mhe. Judith Kapinga
Ameeleza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika hatua nyingine limeendelea na ukarabati mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme ikiwemo ile ya Kihansi, Kidatu pamoja na Ubungo ili kuwezesha Taifa kuwa na umeme wa uhakika muda wote.