Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameuagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuwasimamia Wakandarasi wote wanaojenga na kukarabati miradi ya maendeleo kwa jamii (CSR) hapa nchini ili iweze kukamilika kwa ubora.
Mhandisi Kasekenya, ametoa agizo hilo Mkoani Kigoma leo tarehe 11 Januari, 2025 wakati akikagua miradi ya ujenzi inayoendelea kutekelezwa kwenye Sekta ya Elimu, Afya, Maji na Masoko kwa ushirikiano baina ya Halmashauri za Buhingwe, Manyovu, Kibondo na TANROADS.
Miradi hiyo inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Bweni Buhingwe, Kituo cha mabasi na uzio wa soko Manyovu, Ujenzi wa visima vya maji Buhingwe na Manyovu, Ukarabati wa Hospitali ya Kasulu pamoja na ujenzi wa Hospital Makere na Kibondo.
“Miradi hii inasimamiwa na TANROADS, kwa ushirikiano wa Benki ya Afrika ambayo ilitoa fedha ili kuhakikisha inajengwa kwa viwango vya hali ya juu na kwa wakati ili viweze kutoa huduma kwa wananchi”, amesisitiza Mhandisi kasekenya.
Amefafanua kuwa miradi ya CSR, ni miradi ambayo inajengwa kwa fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii kama vile ujenzi wa visima vya maji, shule, hospitali ambavyo vimetekelezwa kwenye Ujenzi wa barabara ambazo zinaendelea kujengwa Mkoani humo.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, ameahidi kuwa kupitia TANROADS na Wilaya za Buhingwe, Kibondo na Manyovu watashirikiana kuhakikisha Miradi hiyo yote ya CSR inakamilika kwa muda uliopangwa.