Shirika la Afya Duniani, WHO limeomba siku ya Alhamisi Januari 16, 2025 dola bilioni 1.5 kusaidia shughuli zake mnamo mwaka 2025 huku kukiwa na “migogoro ya kiafya ambayo haijawahi kutokea ulimwenguni,” kiasi sawa na mwaka jana.
“Mwaka huu, WHO inatafuta dola bilioni 1.5 kusaidia kazi yetu muhimu katika hali za dharura zinazotukabili na kujibu haraka majanga mapya,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Adhanom Ghebreyesus, wakati wa uwasilishaji wa rufaa hiyo.
WHO, ambayo inafanya kazi katika nchi zaidi ya 150, inakadiria kuwa watu milioni 305 watahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu mwaka huu. Lakini “katika kukabiliana na mahitaji haya yanayoongezeka, tunakabiliwa na changamoto nyingine: pengo linaloongezeka la ufadhili wa misaada ya kibinadamu,” Tedros amebainisha. Hivyo, alieleza, mnamo mwaka 2024, ufadhili wa sekta ya afya duniani hautoshelezi 40% ya mahitaji.
“WHO peke yake haiwezi kushughulikia ukubwa wa changamoto tunazokabiliana nazo. Tunahitaji jumuiya ya kimataifa kushirikiana nasi. Leo, niko hapa kuwaomba muendelee kutuunga mkono,” Bwana Tedros amesema.
Wito huu wa fedha unakuja siku chache kabla ya kuapishwa kwa Donald Trump, ambaye katika muhula wake wa kwanza alizindua utaratibu wa kuiondoa Marekani kutoka kwa WHO, ambayo Washington inasalia kuwa mchangiaji mkubwa zaidi. Waangalizi kadhaa wanahofia kuwa rais mteule wa Marekani atazindua upya utaratibu huo mara moja akiingia Ikulu ya White House.