Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alipiga simu ya video na mwenzake wa China, Xi Jinping, katika ishara ya kuonyesha umoja saa chache baada ya Donald Trump kuapishwa kama rais wa 47 wa Marekani.
Akizungumza kutoka kwenye makazi yake ya Novo-Ogaryovo nje ya Moscow, Putin aliangazia uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili, akisema kwamba uhusiano wao uliegemea kwenye “maslahi ya pamoja, usawa, na manufaa ya pande zote”, akimwita Xi “rafiki mpendwa”.
Moscow imekua ikiitegemea China kama mshirika wa kibiashara na mshirika muhimu wa kidiplomasia huku kukiwa na mzozo kati yake na nchi za magharibi baada ya kuanzisha uvamizi kamili wa Ukraine karibu miaka mitatu iliyopita.
Kwa upande wake, Beijing imetumia mtaji wa kutengwa kwa Urusi kutoka magharibi ili kupata ufikiaji wa upendeleo kwa rasilimali na masoko yake.
Nchi hizo mbili zilitangaza ushirikiano wa “bila kikomo” mnamo Februari 2022 wakati Putin alipotembelea Beijing siku chache kabla ya kutuma makumi ya maelfu ya wanajeshi nchini Ukraine.
Viongozi hao wawili tangu wakati huo wametembelea miji mikuu ya kila mmoja wao mara kwa mara na wamekuwa washirika wa lazima katika lengo lao la pamoja la kuunda upya mpangilio wa kimataifa dhidi ya Magharibi.
Ingawa hakuna kiongozi aliyemtaja Trump moja kwa moja katika sehemu ya runinga ya simu yao, muda wa mazungumzo yao unaweza kuashiria kuwa Putin na Xi wanatarajia kuratibu mbinu yao ya kujihusisha na utawala mpya wa Marekani.