Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 521 katika kipindi cha Julai 1, 2024, hadi Desemba 31, 2024. Hii ni sawa na asilimia 52.2 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, leo Januari 21, 2025, jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji ya Wizara mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Waziri Mavunde amesema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi mzuri, udhibiti madhubuti, na weledi katika ukusanyaji wa mapato kwenye sekta ya madini.
“Wizara imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2015/16 ambapo ilikusanya shilingi bilioni 161 kwa mwaka mzima na mwaka huu ndani ya nusu ya kwanza tayari tumekusanya asilimia 52.2 ya lengo la Shilingi trilioni 1 kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/25”
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameongeza kuwa leseni kubwa na za kati za madini ambazo hazijaendelezwa zitarudishwa Serikalini zitakabidhiwa kwa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kwa ajili ya kuziendeleza kwa manufaa ya taifa.
Aidha, Mavunde amesema kuwa, STAMICO imejipanga kuwa sehemu muhimu ya uzalishaji wa Madini ya Kinywe hapa nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tanzania kuwa kiungo muhimu katika soko la dunia la madini hayo.
Pia, Waziri Mavunde amefafanua kuwa, katika juhudi za Serikali kuwasaidia wakulima wa chumvi nchini, STAMICO itajenga kiwanda kikubwa cha kusafisha chumvi Mkoani Lindi ili kuimarisha soko la wakulima hao na kwa Mitambo ya kiwanda hicho imeshawasili nchini na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Februari 2025.