Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Algeria Mhe. Ahmed Djellal ambaye anamaliza muda wake wa kuhudumu hapa nchini.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika tarehe 22 Januari 2025 ofisini kwake Upanga Jijini Dar es Salaam,Jenerali Mkunda amempongeza Balozi Ahmed Djellal kwa kazi nzuri aliyoifanya nchini, hususani kudumisha ushirikiano baina ya JWTZ na Jeshi la Algeria katika nyanja ya mafunzo, mazoezi na kubadilishana uzoefu wa kijeshi.
Aidha, Mkuu wa Majeshi ameomba ushirikiano baina ya majeshi haya mawili kuendelea kudumishwa ili kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za kijeshi.
Naye Balozi Ahmed Djellal ambaye alifika ofisini kwa Mkuu wa Majeshi kumuaga baada ya kumaliza muda wa uwakilishi nchini Tanzania, amelishukuru JWTZ kwa ushirikiano aliopatiwa kwa kipindi chote alichohudumu hapa nchini, na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya majeshi ya nchi hizi mbili katika mafunzo,mazoezi na kubadilishana uzoefu wa Kijeshi.
Uhusiano uliopo baina ya majeshi haya mawili ni muendelezo wa mahusinao ya muda mrefu baina ya Tanzania na nchi ya Algeria katika masuala mbalimbali ya kidiplomasia tangu kuasisiwa kwake.