Bunge la Iraq inaripotiwa kupitisha sheria kadhaa, ikiwemo ile itakayoruhusu ndoa za watoto wa kike wakiwa na umri wa miaka tisa na kwa mujibu wa Mail Online, marekebisho ya sheria hiyo ya Iraq yataipa mahakama za Kiislamu mamlaka zaidi juu ya masuala ya kifamilia, ikiwa ni pamoja na ndoa, talaka, na urithi.
Sheria za sasa za Iraq zinaweka umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18 katika hali nyingi, lakini mabadiliko hayo yaliyopitishwa Jumanne, Januari 21, yatatoa nafasi kwa viongozi wa kidini kuamua kulingana na tafsiri yao ya sheria za Kiislamu.
Baadhi ya tafsiri hizi huruhusu ndoa za watoto wa kike wakiwa katika umri wa miaka ya mwanzo ya balehe au hata miaka tisa chini ya madhehebu ya Ja’afari, ambayo yanatumiwa na viongozi wengi wa kidini wa Kishia nchini Iraq.
Wafuasi wa mabadiliko hayo, ambao kwa kiasi kikubwa ni wabunge wa Kishia wa kihafidhina, wanayatetea kama njia ya kuendana na kanuni za Kiislamu na kupunguza ushawishi wa Magharibi kwenye utamaduni wa Iraq.
Hata hivyo, Intisar al-Mayali, mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanachama wa Ligi ya Wanawake ya Iraq, alisema kupitishwa kwa marekebisho ya sheria ya hali ya kiraia ‘kutaleta athari mbaya kwa haki za wanawake na watoto wa kike kupitia ndoa za mapema’.
Kikao cha bunge kilichoshuhudia kupitishwa kwa marekebisho hayo kilimalizika kwa vurugu na shutuma za ukiukaji wa taratibu.