HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imetoa Sh bil 2.6 kwa vikundi 315, ikiwa ni mikopo ya asilimia 10 ambayo ni mpango wa serikali wa kuinuia wananchi wake kiuchumi.
Akikabidhi fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani amewataka maofisa maendeleo ya jamii na biashara mkoani humo kuwasaidia wananchi kuchagua biashara zenye manufaa na ambazo wana ujuzi nazo ili waweze kunufaika na fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali.
Dk Batilda alikabidhi fedha hizo jana wakati wa uzinduzi wa utoaji wa mikopo hiyo inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ngazi ya mkoa uliofanyika katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Alisema lengo la mikopo hiyo ni kuhakikisha wananchi wanainuka kiuchumi, hivyo ipo haja ya maofisa hao kuwasaidia wananchi kuchagua fursa za biashara ambazo zitakuwa endelevu na zenye tija kwao.
“Licha ya kuhimiza vikundi kuchangamikia fursa ya mikopo kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo, wasaidieni katika kuchagua biashara zenye manufaa na si kuiga biashara za wengine ambazo hawana elimu au ujuzi nazo,” aliongeza Batilda.