Waziri Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Januari 23,2025 amekutana na uongozi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya huduma za Afya ya nchini Korea na kuuelezea kuwa katika kipindi cha miaka mitano (5), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imenufaika na ushirikiano wa pamoja kati yake na Korea kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP-IV) pamoja na Mpango Mkakati wa Tano.
Pia wamejadili mambo yanayohusu Sekta ya Afya ikiwemo kuimarisha huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika mikoa ya Pwani na Dodoma.
Tanzania na Korea zimeazimia kuendelea kujenga uwezo kwa Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma juu ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, mpango wa kiufundi wa usimamizi wa hospitali sambamba na ukarabati na ujenzi wa wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa (NICU).
“Kwa sababu hiyo, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Korea pamoja na taasisi ya (Korea Foundation for International Healthcare, KOFIH) kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania, hususan katika sekta ya afya,” amesema Waziri Mhagama