KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeipongeza Tume ya TEHAMA kwa juhudi inazofanya katika kukuza sekta hiyo nchini, lakini zaidi katika jitihada za `kukiuza’ Kiswahili duniani.
Pongezi hizo zimetolewa bungeni jijini Dodoma jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso wakati kamati yake ilipokuwa inapokea taarifa ya utekelezaji ya Tume ya TEHAMA iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Dk. Nkundwe Mwasaga.
Katika wasilisho lake, Dkt. Mwasaga aligusia mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana ndani ya Tume, mojawapo likiwa kufanikiwa kuingia makubaliano na Kampuni ya ALMAWAVE ya Italia inayojihusisha na uandaaji wa lugha ya Kiswahili itakayowezesha mifuno ya akili unde kuweza kuwasiliana kama binadamu.
Alisema kampuni hiyo itashirikiana na Tume ya TEHAMA na taasisi mbalimbali nchini kuanzisha Swahili Large Language Model (LLM) ambayo itawezesha ukuaji wa lugha ya Kiswahili kwenye tasnia ya akili unde duniani.
“Hili litasababisha ukuaji wa fursa kwa wananchi wa Tanzania kutumia lugha ya Kiswahili kwa kutengeneza bunifu kwenye sekta mbalimbali za uchumi wa Tanzania, Afrika na duniani kote. Hili litakuza sana soko la Kiswahili na kuimarisha uchumi wa kidijitali wa Tanzania,” alisema Dkt. Mwasaga.
Makubaliano ya ushirikiano yalisainiwa mwaka 2024 wakati wa Kongamano la Nane la TEHAMA nchini (TAIC 2024) jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo la kila mwaka, kwa mwaka jana lilivutia washiriki zaidi ya 4,000 wa ndani na nje ya nchi kama vile Marekani, Umoja wa Mataifa, UNESCO, UNICEF, Umoja wa Ulaya (Estonia, Finland, Italia, Ujerumani, Uturuki, na Ubelgiji), Afrika Kusini, Umoja wa Afrika, Nchi za Afrika Mashariki, Urusi, India, na China.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Kakoso, alionesha furaha kwa taarifa hiyo, akisema; “Tukumbatie hizi fursa. Tuna mtaji mkubwa wa watu nchini ambao ni soko kubwa. Tunaweza kuona ni kama kitu kidogo sana, lakini wenzetu wa nchi jirani wananufaika sana kupitia Kiswahili. Tunaozungumza Kiswahili fasaha ni sisi, lakini wanaonufaika zaidi kupitia lugha ya Kiswahili ni wengine. Tuseme Hapana.
“Hili mkalisimamie hili kwa lengo la kuhakikisha Kiswahili kinaleta faida zaidi kwa nchini,” alisema Mhe. Kakoso.