Shirika la Haki Elimu, kwa kushirikiana na serikali ya Canada kupitia taasisi ya Global Affairs Canada, limezindua Mradi wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia katika Elimu (MMUKE). Mradi huu utagharimu Dola za Canada Milioni 4.5 (takribani Shilingi Bilioni 7.8 za Kitanzania).
Lengo lake kuu ni kuboresha mazingira ya elimu, hasa kwa wasichana, kwa kuhakikisha miundombinu bora ya maji na usafi wa mazingira, pamoja na kupunguza ukatili wa kingono na kijinsia.
Akizungumza katika uzinduzi wa kitaifa uliofanyika katika shule ya Sekondari Buna Korogwe, Mkurugenzi wa Haki Elimu, Dkt. John Kalage, alisema mradi huo una malengo ya kujenga mazingira salama yanayozingatia mahitaji ya kijinsia katika shule.
Pia unalenga kuimarisha ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kuhakikisha shule zinakuwa na vifaa safi na salama vya usafi vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi wa jinsia zote.
“Mradi huu utatekelezwa katika shule 40 (16 za msingi na 24 za sekondari) katika wilaya nane za mikoa minane ya Tanzania Bara: Korogwe (Tanga), Mkuranga (Pwani), Kilosa (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma), Babati (Manyara), Iramba (Singida), Muleba (Kagera), na Musoma (Mara).
Hata hivyo takiribani wanafunzi 24,000, wakiwemo wasichana 12,240 na wavulana 11,760 wenye umri wa miaka 10 hadi 19, pamoja na walimu 100 na wajumbe 16 watafikiwa na mradi pamoja na vikundi vya Marafiki wa Elimu” amesema Dkt Kalage
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. William Mwakilema, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, amewaagiza wataalamu kushirikiana na wahusika kuhakikisha mradi unafanikiwa. Pia na kuwasisitiza watendaji wa shule na halmashauri kulinda na kutunza miundombinu na vifaa vitakavyotolewa kupitia mradi huo.