Halmashauri ya Jiji la Arusha imefanikiwa kununua mitambo mipya mitatu yenye thamani ya Sh1.7 Bilioni kwa ajili ya ukarabati wa barabara za ndani.
Mitambo hiyo iliyozinduliwa leo january 28,2025 na Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranghe ni Grader aina ya Catapiler -Model 140GC pamoja na Malori mawili (SINOTRUK-ModI HOWO) iliyonunuliwa kwa fedha ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha 2024/25.
Akizungumza katika ghafla ya uzinduzi wa mitambo hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo amesema mitambo hiyo inakwenda kujibu kilio cha muda mrefu cha wananchi ikiwemo Changamoto ya barabara korofi hasa zinazoharibiwa na mvua.
Alisema halmashauri hiyo ilitenga kiasi cha Shilingi billion mbili kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na malori.
“Kwa neema ya mungu tumeweza kununua nyenzo hizo kwa thamani ya Sh1.7 billion na fedha zilizobaki zitagawanywa kwa kila kata kiasi cha Shilingi milioni nne kwa ajili ya ununuzi wa vifusi” amesema na kuongeza;
“Madiwani wangu walikuwa kwenye wakati mgumu sana kwa tatizo la ubovu wa barabara, tena wengine waliburuzwa kwenye matope ila kwa sasa madiwani wangu tembeeni vifua mbele hakuna diwani atakayepata shida tena” amesema Kayombo.
Awali mhandisi wa jiji hilo, Jacob Mwakiambiki amesema kuwa Mitambo na Malori hayo mawili yamenunuliwa kwa fedha za ndani baada ya halmashauri hiyo kutenga kiasi cha shilingi billion mbili kupitia bajeti yake ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/25.
“Ndani ya mwaka huu wa fedha jiji la Arusha limefanikiwa kununua mtambo mmoja (Grader) aina ya Catapiler -Model 140GC pamoja na Malori mawili (SINOTRUK-ModI HOWO) kwa ajili ya kutatua ukarabati na matengenezo ya barabara za ndani” amesema.
“Catapiler ni shilingi 1,329270,000.00 na gharama za Malori mawili ni shilingi 413,250,004.70, pamoja na VAT” amesema.
Nae Meya wa Jiji la Arusha, amewataka wananchi na madiwani kutunza mitambo hiyo ili iweze kudumu na kufanya kazi iliyokusudiwa.
” Naomba jamani tutunze mitambo hii na tusikubali kunyamaza pale tunapoona inachepushwa kufanya kazi isiyo ya malengo yetu kwani Arusha tunakwenda kutangaza sasa kero ya barabara imekwisha na kuwa na hadhi ya Jiji la kitalii” amesema.
Diwani wa kata ya Muriet, Francis Mbise amesema kuwa kero ya barabara ndani ya Jiji la Arusha ni changamoto kubwa sana hivyo wanaishukuru serikali kuridhia kupitishwa kwa bajeti ya ununuzi wa mitambo hiyo.
Naye Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Arusha, Willfred Soilel Mollel aliishukuru halmashauri hiyo kwa kutekeleza ilani ya ccm na kununua mitambo hiyo kwa ajili ya matengenezo ya barabara korofi alisema itasaidia kuwapunguzia kero ya marabara ambazo hazipo kwenye mpango wa Tarura.
Aliitaka halmashauri hiyo kuhakikisha mitambo hiyo inaanza kazi mara moja hasa kata za pembezoni ambazo kuna changamoto kubwa ya ubovu wa barabara.