Rais Donald Trump ametoa agizo la kusitisha utoaji wa mikopo na ruzuku zote za Serikali kuu ya Marekani hatua ambayo inatarajiwa kuathiri Sekta muhimu kama Elimu, Afya, Makazi na misaada ya maafa Nchini humo.
Hatua hii imeibua wasiwasi miongoni mwa Viongozi wa Serikali za mitaa na Mashirika yasiyo ya kiserikali wakihofia athari za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na kusitishwa kwa fedha hizo pia Wakosoaji wanasema kuwa hatua hii inaweza kusababisha kusimama kwa huduma muhimu zinazotegemea ruzuku na mikopo ya Serikali kuu.
Kwa upande wake Ikulu imetetea uamuzi huo kupitia Ofisi ya Usimamizi na Bajeti ikisema kuwa hatua hiyo inalenga kufanya mapitio ya kina ya matumizi ya fedha za Serikali na kuhakikisha kuwa zinaendana na vipaumbele vya utawala wa Rais Trump.
Hata hivyo Mawakili Wakuu wa Serikali kutoka majimbo kadhaa wametangaza mpango wa kufungua kesi kupinga hatua hiyo wakidai kuwa itaathiri vibaya maisha ya Wananchi wa kawaida hasa wale wanaotegemea huduma za kijamii zinazofadhiliwa na Serikali kuu.
Wakati mjadala ukiendelea Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa hatua hii ni sehemu ya juhudi za utawala wa Trump kupunguza matumizi ya Serikali na kuelekeza rasilimali kwenye vipaumbele vingine vya kiutawala.