Watumishi wa afya mkoani Tanga wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uchangiaji damu pamoja na kutoa elimu ya afya kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya afya nchini.
Zoezi hilo lililofanyika katika viwanja vya Lamore liliwaleta pamoja madaktari, wauguzi, maafisa afya, na wahudumu wa hospitali mbalimbali mkoani humo. Mbali na uchangiaji wa damu, wananchi walipata fursa ya kupima afya zao bure, ikiwa ni pamoja na vipimo vya shinikizo la damu, sukari, VVU, uzito na urefu, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu lishe bora na afya ya uzazi.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi hilo, mgeni rasmi wa tukio hilo, ambaye ni Mwenyekiti wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM ) Mkoa wa Tanga, Ramadhani Omary, aliwapongeza wahudumu wa afya kwa hatua hiyo na kusema kuwa ni kitendo cha kijasiri na cha kiungwana. Alisema kuwa ni jambo la kufurahisha kuona wataalamu wa afya wakijitoa kwa jamii na pia kuthamini juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya afya.
“Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anajitahidi kuboresha huduma za afya nchini. Nimesikiliza risala yenu na kuona kuwa mmeamua kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Katika uchaguzi wa mwaka 2025, hongereni sana kwa uamuzi huo. Kwetu sisi ni faraja, na hata kwake yeye ni faraja kuona wataalamu wa sekta ya afya wakieleza mafanikio na maendeleo yaliyofanyika,” alisema Omary.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Afya na Maendeleo la Umoja wa Wahudumu wa Afya, Madaktari na Manesi wa Mkoa wa Tanga, Bw. Mwinyiusi Shekwepashua, alisema kuwa lengo kubwa la tukio hilo ni kuonyesha mshikamano na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya. Alisema kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.
“Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kujenga hospitali mpya za rufaa za wilaya, vituo vya afya katika kila kata, na zahanati nyingi zaidi vijijini. Hii imeongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi na kupunguza vifo vitokanavyo na ukosefu wa huduma za dharura,” alisema Shekwepashua.
Aliendelea kueleza kuwa, mbali na uboreshaji wa miundombinu, serikali imeongeza ajira kwa watumishi wa afya, hatua ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa wahudumu wa afya katika hospitali na vituo vya afya nchini.
“Kwa kipindi cha serikali ya awamu ya sita, serikali imefanikiwa kuongeza ajira kwa watumishi wa afya, kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hasa katika hospitali za wilaya na vituo vya afya. Hatua hii imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya,” aliongeza.
Katika zoezi hilo, jumla ya unit 112 za damu zilichangishwa, huku zaidi ya watu 255 wakijitokeza kupima afya zao. Madaktari walieleza kuwa uchangiaji wa damu ni muhimu kwa sababu inasaidia wagonjwa wanaopata upasuaji, akina mama wajawazito wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, na wahanga wa ajali wanaohitaji damu kwa dharura.
Zoezi hilo lilihitimishwa kwa kauli ya pamoja ya wahudumu wa afya wa Mkoa wa Tanga kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinazidi kuimarika na kuwafikia wananchi wote kwa wakati.